Mgahawa aliotumia Rais John Magufuli kupata mlo wa mchana na msafara wake juzi kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza, umekuwa kivutio kwa wateja wengi wakinunua chakula na kutaka kukalia kiti na meza alivyotumia kiongozi huyo.
Meneja wa mghahawa huo wa Victoria, Elizabeth Maneno (pichani) alisema jana kwamba hali hiyo ilijitokeza mara baada ya Rais kuondoka hapo.
“Hata leo tumepokea wateja wengi kulinganisha na siku nyingine,baadhi yao wanaagiza chakula kwa sharti la kutaka kukikalia kitina meza aliyotumia Rais Magufuli,” alisema Elizabeth.
Akizungumzia hali ilivyokuwa juzi kabla na wakati wa ugeni huo meneja huyo alisema: “Ilikuwa ni hofu na woga uliochanganyika na furaha kumwona Rais akiingia kwenye mgahawa wetu wa chai ya rangi ya Sh200 na ya maziwa Sh300.
“Mshtuko wetu uligeuka furaha baada ya kubaini kuwa oda ya sahani 28 za kubeba (takeaway), tulizoagizwa mapema asubuhi bila kuelezwa zinakoenda zilikuwa za ujumbe wa Rais,” alisema na kuongeza:
“Kabla Rais Magufuli hajaingia kwenye mgahawa wetu, alikuja mtu mmoja tusiyemfahamu na kuagiza sahani 28 za chakula kwa gharama ya Sh5,000 kila moja,”
Alisema baada ya kumtaarifu mteja wake kuwa chakula kiko tayari, alielekezwa kuandaa meza na viti kwa sababu wageni wake (wa mteja), sasa wameamua kula palepale mgahawani.
“Ghafla tulimwona Rais anaingia ndani ya mghahawa wetu; kwanza tulishikwa hofu, woga na kihoro tusijue tufanye nini hadi tulipogutushwa na aliyetoa oda kwa kutuagiza tugawe chakula alichoagiza,” alisema meneja huyo; “hapo ndipo tulipobaini kumbe chakula kile kilikuwa cha ugeni wa Rais.”
Pamoja na chai ya rangi na ya maziwa, mghahawa huo pia unauza vyakula vya aina mbalimbali kwa bei kati ya Sh1,500 hadi Sh5,000 kwa vyakula vya kubeba, huku soda ikiuzwa kwa Sh500 kwa chupa.