Askari wa Kikosi cha Zimamoto, Manispaa ya Shinyanga wamenusurika kipigo kutoka kwa wananchi wa mtaa wa Banduka, kata ya Ndala mjini hapa, baada ya kuchelewa kufika kwenye tukio la nyumba kuungua moto ikiwa na watoto ndani yake.
Baadhi ya mashuhuda walidai kuwa moto huo ulianza kuwaka kwenye nyumba ya Azizi Abdallah, saa 2:00 asubuhi na uliunguza baadhi ya vitu kwenye nyumba hiyo ambayo wanaishi wapangaji pekee kwa kile kinachosadikiwa kuwa ni hitilafu ya umeme ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara.
Mmoja wa walioshuhudia, Onesmo Shija, alisema wapangaji wote walikuwa wamekwenda makazini na kubaki watoto ambapo saa 2:00 aliona moshi ukifuka kwenye madirisha huku watoto wakipiga kelele, ndipo walipokusanyika na kuanza kuuzima na kuwanusuru kifo watoto hao.
Shija alisema baada ya wananchi kutoa taarifa mapema kwa kikosi hicho, walichelewa kufika na walipofika tayari moto ulikuwa umeshazimwa ndipo wananchi walipopandwa hasira na kuanza kuokota mawe na kuwashambulia lakini mwenyekiti wa mtaa aliwazuia.
Mwenyekiti wa mtaa huo, Terege Nyankangara alisikitishwa na kikosi cha Zimamoto kuchelewa kufika eneo la tukio na kueleza uchelewaji huo ulitaka kuhatarisha amani. Hata hivyo, Nyankangara aliwaasa wananchi wake kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.
Askari wa kikosi cha Zimamoto, Omari Magea alikiri wananchi hao kutaka kuwashambulia kwa mawe na alishukuru Mwenyekiti wa mtaa kuwezesha kurejesha amani. Alisema kilichowachelewesha ni uhaba wa vitendea kazi.
Aidha msimamizi wa nyumba hiyo, Daudi Nyanda alisema nyumba hiyo wanaishi wapangaji 10 na hakuna aliyepata madhara zaidi ya mali zao kuteketea. Alisema thamani bado haijafahamika.
0 comments:
Post a Comment