Latest News
Loading...

Bajeti ya Serikali 2016/ 2017 ni Trilioni 29.5.....Matumizi ya Kawaida ni Trilioni 17.7, Mikopo ni Trilioni 11.1. Bofya Hapa Kuona Vipaumbele Vilivyotajwa

Bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano itaizidi ya Serikali ya Awamu ya Nne kwa Sh7.1 trilioni baada ya Waziri wa Fedha kutangaza sura ya bajeti ya mwaka 2016/17 inayoonyesha kutakuwa na makusanyo na matumizi ya Sh29.5 trilioni.

Sura hiyo ya bajeti ya mwaka 2016/17 inatofautiana na iliyopita iliyokuwa ya Sh22.45 trilioni katika maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na kiwango cha fedha kitakachotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo, ambacho ni zaidi ya mara mbili ya fedha za eneo hilo katika bajeti iliyopita.

Waziri wa Fedha, Dk Phillip Mpango alisema wakati akiwasilisha mapendekezo ya kiwango cha ukomo wa bajeti jijini Dar es Salaam jana kuwa kati ya fedha hizo, Sh18.46 trilioni, ambazo ni sawa na asilimia 62.5 ya bajeti yote, zitatokana na jumla ya mapato ya ndani yanayohusisha na halmashauri.

Kiwango hicho kimezidi Sh3.64 trilioni ya bajeti iliyopita ambayo ililenga kukusanya Sh14.82 trilioni.

“Kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Sh15,105 bilioni, sawa na asilimia 82 ya mapato ya ndani,”alisema Dk Mpango.

Alisema makisio ya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi yameongezeka kwa kuwa kuna viashiria vingi vinavyoonyesha kwamba Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa kushirikiana na wizara na taasisi zinazokusanya maduhuli, zina uwezo wa kukusanya kiasi hicho.

Alisema: “Kipaumbele cha kwanza cha Serikali kitakuwa ni kujizatiti katika ukusanyaji wa mapato kwa kubuni vyanzo vipya na kuendelea kudhibiti mianya mbalimbali ya ukwepaji wa kodi. Suala hili linahitaji ushirikiano wa karibu na wananchi ili tujiletee maendeleo ya haraka kwa kushiriki kulipa kodi na kuwafichua wakwepa kodi kwa kuwaona kama maadui wa maendeleo yetu.”

Kwa mujibu wa Dk Mpango, Sh17.72 trilioni zitakuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, wakati Sh11.82 trilioni, sawa na asilimia 40 ya bajeti nzima, zimetengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Katika bajeti iliyopita, matumizi ya kawaida yalitengewa Sh16.7 trilioni, sawa na asilimia 74.3 wakati shughuli za maendeleo zilipangiwa Sh5.76 sawa na asilimia 25.9.

“Asilimia 40 kwenda kwenye mipango ya maendeleo, hili ni jambo jema,” alisema Freeman Mbowe, ambaye ni mwenyekiti wa Chadema na kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, alipoongea na waandishi.

“Kwamba tumepunguza matumizi ya kawaida ya Serikali na kuelekeza fedha zaidi kwenye mipango ya maendeleo, nasema hili ni jambo jema kama litatekelezeka.” 

Vipaumbele 
Kwa mujibu wa Dk Mpango, shughuli zitakazopewa kipaumbele kwenye mipango hiyo ya maendeleo zimegawanywa katika maeneo manne ambayo ni viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, kufungamanisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu, mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji na pia usimamizi wa utekelezaji wa mpango.

Dk Mpango alisema washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh3.6 trilioni, ikiwa ni ongezeko la Sh1.7 trilioni kulinganisha na Sh1.88 trilioni zilizokuwa zinategemewa kwenye bajeti iliyopita.

Fedha hizo zitakuwa za misaada na mikopo nafuu kutoka nje ambayo ni pamoja na GBS, Basket Fund na miradi ya maendeleo.

Aidha Serikali inatarajia kukopa Sh5,374.3 bilioni kutoka soko la ndani kwa ajili ya kulipia hati fungani na dhamana za Serikali zinazoiva pamoja, wakati kutoka kwenye soko la nje kwa masharti ya kibiashara inatarajia kukopa Sh2.1 trilioni.

Awali Spika Job Ndugai alisema kwa mujibu wa utaratibu mapendezo hayo yalipaswa kuwasilishwa tangu Machi 11, lakini kutokana na ratiba za wabunge wengi kuwa kwenye majimbo yao, aliamua kuongeza siku.

“ Sasa ninawashauri wabunge wote kwenda kuyasoma mapendekezo hayo vyema ili mpate nafasi ya kuchangia fedha bajeti itakapowasilishwa bungeni. Pia mhudhurie kwenye vikao vya kamati zenu ili kujipanga vyema. Wale watakaokuwa hawaonekani kwenye vikao, tutawasilisha majina yao kwenye vyama vyao ili wachukuliwe hatua zinazostahili.”

Miradi ya maendeleo 
Katika kuongeza wigo wa makusanyo ya kodi, Dk Mpango alisema sera za mapato kwa mwaka 2016/2017 itajielekeza kufanya tathimini ya mkupuo ya majengo ili kuongeza mapato.

Katika mpango wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, Dk Mpango alisema kipaumbele kitakuwa ni mradi wa magadi soda ulioko kwenye Bonde la Engaruka ambako utafiti umebaini kuna magadi ya mita za ujazo bilioni 4.68 ambazo huongezeka kila mwaka kwa mita milioni 1.9 za ujazo.

“Mradi utahusisha kiwanda cha kuzalisha tani milioni moja za magadi kwa mwaka kwa ajili ya matumizi ya viwanda, hususan madawa, vioo na sabuni,” alisema.

Mradi huo utakapokamilika utaliingizia taifa Sh 400 bilioni kwa mwaka.

Eneo jingine ni kufufua kiwanda cha General Tyre cha Arusha, ambacho kimetengewa Sh2 bilioni kwa kazi hiyo. Pia kiwanda cha viuadudu kilichopo Kibaha mkoani Pwani ambacho mradi wake utatekelezwa kwa awamu tatu, mbili za mwisho zikihusisha ujenzi wa kiwanda cha mbolea na cha virutubisho.

Pia mpango huo utahusisha uendelezaji wa viwanda vidogo mkoani Morogoro, Dar es Salaam, Mbeya na Mwanza.

Katika kufunganisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu, Serikali itaweka nguvu kwenye elimu na mafunzo ya ufundi, ikihusisha kuimarisha mifumo, majengo na miundombinu katika shule za awali, msingi na sekondari.

Pia itahusisha ukarabati, upanuzi na ujenzi wa vyuo vikuu, mradi wa upanuzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (Mkwawa, Duce, Udom na OUT, Ardhi, Mzumbe, Sokoine, Muhimbili, Ushirika, Chuo Kikuu cha Sayansi cha Mwalimu Nyerere na pia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Eneo hilo litahusisha uendelezaji ustawi wa jamii kwa kuangalia huduma za afya, maji, kazi na ajira, na uwezeshaji wananchi kwa kutoa Sh50 milioni kwa kila kijiji.

Mazingira wezeshi 
Katika kujenga mazingira wezeshi, Serikali itaongeza uwezo wa uzalishaji umeme, usambazaji umeme mijini na vijijini, ujenzi wa kiwanda cha kupokea, kuchakata na kubadilisha gesi asilia kuwa katika kimiminika kwa ajili ya kusafirisha nje, ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha gesi asilia, ujenzi wa miundombinu ya usafiri, teknolojia ya habari na mawasiliano, miradi ya makaa ya mawe na mradi wa chuma wa Liganga.

0 comments:

Post a Comment