Home »
KITAIFA
» David Kafulila Apewa Saa Moja Kubadili Hati ya Kiapo Kesi ya Kupinga Matokeo ya Uchaguzi
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora imetoa uamuzi mdogo katika kesi iliyofunguliwa na David Kafulila kupinga matokeo ya ubunge Jimbo la Kigoma Kusini kwa kuutaka upande huo wa mlalamikaji kulipa gharama kwa upande wa mjibu maombi pamoja na kuandaa hati ya kiapo upya ndani ya saa moja.
Uamuzi huo mdogo ulitolewa jana na Jaji wa Mahakama hiyo, Ferdinard Wambali, baada ya upande wa mjibu maombi ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Juma Masanja kwa kushirikiana na wakali wa kujitegemea, Kennedy Fungamtama, kuweka pingamizi kuwa hati ya kiapo ya Kafulila isipokelewe kwa sababu haikukidhi matakwa ya sheria.
Awali, Jaji Wambali aliwauliza mawakili wa pande zote kama wako tayari kusikiliza uamuzi mdogo wa pingamizi la hati ya Kafulila isipokelewe mahakamani kwa sababu haikukidhi matakwa ya sheria.
Upande wa mlalamikaji (Kafulila) ukiongozwa na mawakili watatu, Prof. Abdallah Safari, Danieli Rumenyela na Ingatus Kagashe na upande wa wajibu maombi ukiongozwa na Wakili wa Kujitegemea Kennedy Fungamtama na Wakili wa Serikali Mwandamizi Juma Masanja na Wakili wa Serikali Fred Nyamkumbo, wote walikubali.
Akitoa uamuzi huo mdogo, Jaji Wambali alisema: “Nimepitia mapingamizi mawili yaliyotolewa na upande wa wajibu maombi kutokana na mabishano ya kisheria ya mawakili wa pande zote, mahakama hii imeamua kwamba upande wa mleta maombi (Kafulila) watalipa gharama tangu pale kesi hiyo na hati yake ya kiapo irekebishwe ndani ya saa moja na kesi itaendelea tena mahakamani saa 5:30 asubuhi (jana),” alisema.
Jaji Wambali aliahirisha kesi hiyo saa 4:00 asubuhi kwa ajili ya kulekebishwa hati hiyo ya kiapo kabla ya kuendelea kusikiliza shahidi wa kwanza upande wa mleta maombi.
Katika kesi hiyo Kafulila (NCCR-Mageuzi) anapinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge Jimbo la Kigoma Kusini yaliyompa ushindi Mbunge wa jimbo hilo, Hasna Mwilima (CCM).
0 comments:
Post a Comment