Latest News
Loading...

Maalim Seif leo kutangaza msimamo wa CUF Zanzibar


Wakati joto la kuundwa Baraza la Mawaziri Zanzibar likiwa linaendelea kupanda bila ya Chama cha Wananchi (CUF) kuwamo katika serikali, Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, leo anatarajiwa kutoa mwelekeo wa kisiasa wa chama chake baada ya kususia uchaguzi mkuu wa marudio visiwani humu.

Msimamo huo wa CUF kuhusu mwelekeo wa Chama baada ya kugomea uchaguzi mkuu, unakuja baada ya kukamilika vikao vizito vya chama hicho kikiwamo cha Kamati Tendaji na Baraza Kuu la Uongozi vilivyofanyika Shangani Mjini Zanzibar.

Akizungumza toka mjini Zanzibar jana, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe, alisema kuwa tamko la chama hicho litatolewa na Katibu Mkuu wa CUF baada ya kukamilika kwa vikao muhimu vya chama hicho.

Alisema vikao hivyo vimefanyika kwa siku nne vikitanguliwa na vikao vya siku mbili vya Kamati Tendaji vilivyofanyika chini ya Mwenyekiti wake, Maalim Seif.

“Vikao vimekamilika salama na ajenda kubwa tulikuwa tunajadili hali ya kisiasa ya Zanzibar baada ya kufanyika uchaguzi mkuu wa marudio kinyume cha Katiba na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar,” alisema Shehe.

Hata hivyo, alisema maazimio ya kikao hicho yatatangazwa na Maalim Seif ili wanachama na wananchi kwa jumla, wafahamu msimamo wa chama hicho.

Alisema mwelekeo wa CUF kisiasa utaendelea kubakia kupigania haki ya wananchi iliyoporwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, baada ya kufuta matokeo kinyume cha Katiba na Sheria Oktoba 28, mwaka jana.

Aidha, alisema Kikao cha Baraza Kuu kilikuwa cha kwanza kufanyika tangu kilipopitisha azimio la chama la kususia uchaguzi mkuu wa marudio uliyofanyika Machi, mwaka huu.

Msimamo wa Baraza Kuu la CUF umesababisha chama hicho kupoteza viti vyote vya Uwakilishi katika Majimbo 54 na Wadi 111 za madiwani katika Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na kupoteza nafasi ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Hata hivyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alisema kuwa anaamini Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, atatumia hekima na busara kwa kutumia nafasi zake 10 za Kikatiba kuwateua viongozi wa vyama vingine kuwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa madhumuni ya kuendeleza Serikali Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK).

Hata hivyo, nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar iliyokuwa ikishikiliwa na Maalim Seif, imekwama kufanyika uteuzi wake baada ya vyama vilivyoshiriki uchaguzi wa marudio, kushindwa kufikia masharti ya Katiba ikiwamo kupata asilimia 10 ya matokeo ya kura za Rais au viti vya majimbo katika Baraza.

Azimio la CUF linasubiriwa kwa hamu kubwa na wananchi wa Zanzibar kama dira ya mwelekeo wa hali ya kisiasa ya Zanzibar baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa marudio wakati Rais Dk. Shein akiendelea kukamilisha kupanga safu za uongozi wa serikali yake.

0 comments:

Post a Comment