Latest News
Loading...

Serikali Kupitia Upya Mikataba ya Shirika la Reli Tanzania (TRL)


Serikali imeliagiza Shirika la Reli Tanzania (TRL), kupitia upya mikataba ya ununuzi wa vichwa vya treni na mabehewa ili kubaini kasoro zilizojitokeza na kuchukua hatua stahiki kabla ya maboresho ya reli ya Tanga-Moshi-Arusha.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa agizo hilo mkoani Kigoma wakati akikagua miundombinu ya reli na kusissitiza nia ya serikali kufufua reli ya kanda ya kaskazini ili kuimarisha huduma ya uchukuzi katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha.

“Kama Serikali tumewekeza vya kutosha katika TRL, hivyo tunawataka mfanye biashara itakayolipa nasi tutahakikisha popote reli ilipo inatoa huduma iliyokusudiwa na kuchangia kukuza uchumi wa nchi”,amesema Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa amewataka wafanyakazi wa TRL kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kupata bidhaa na abiria wengi wa kuwasafirisha nchini kote.

Amesema Serikali imedhamiria kuliongezea nguvu TRL ambapo baadhi ya mitambo kutoka Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) itakabidhiwa kwa shirika hilo hivyo kulitaka kuwa na mpango madhubuti wa kufanya biashara na kurudisha hadhi ya usafiri wa reli hapa nchini.

“Fanyeni bidii ili mpate mzigo wa kusafirisha kutoka Tanga kwenda Moshi na Arusha ili kufikia lengo la kubeba mzigo wa tani milioni moja kwa mwaka”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Amezungumzia umuhimu wa TRL kuafanya kazi kwa karibu na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA), ili kuongeza kasi ya huduma za uchukuzi nchini, kuongeza fursa za ajira na kukuza pato la shirika na taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TRL, Bw. Masanja Kadogosa amesema TRL imejipanga kutafuta masoko ndani na nje ya nchi ili kuboresha huduma za uchukuzi na kukuza pato lake.

Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua Meli ya MV Liemba na kuitaka Mamlaka ya Usimamizi wa usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), kuhakikisha meli za MV Liemba na MV Mwongozo zinakaguliwa na kufanya kazi inavyostahili katika Ziwa la Tanganyika.

“Tumieni fursa ya kuwa karibu na nchi za maziwa makuu kufanya biashara ili meli zetu zipate mzigo wa kutosha na kuongeza mapato kwa taifa”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa ambaye yupo katika ziara mkoani Kigoma amewataka viongozi na wafanyakazi wa taasisi zilizo chini ya wizara yake kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuibua fursa za kiuchumi katika ukanda wa magharibi na hivyo kufufua miundombinu itakayochochea uchumi wa mikoa ya magharibi mwa Tanzania yenye fursa nyingi za kibiashara.

Imetolewa na :
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

0 comments:

Post a Comment