Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji (PIC) imeshtushwa baada ya kubaini Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilitumia Sh18 bilioni mwaka 2013/2014 kwa ajili ya mafunzo, semina na warsha.
Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Lolesia Bukwimba alisema matumizi ya fedha hizo ni makubwa ikilinganishwa na kazi iliyofanywa na mamlaka hiyo kwa mwaka huo wa fedha.
Alisema wakati mapato ya TCRA kwa mwaka huo yalikuwa Sh79 bilioni, gharama za uendeshaji zilikuwa Sh76 bilioni.
“Hii ina maana fedha zilizopelekwa Hazina zilikuwa kidogo. Kama mamlaka ingepunguza matumizi, Serikali ingepata mapato ya kutosha,” alisema.
Bukwimba alisema hilo ni tatizo na kamati hiyo itatoa maagizo kwa mamlaka hiyo Jumamosi ijayo itakapoitembelea.
“Kuna mambo mengi ya kitaalamu ambayo tunahitaji kuona shughuli zake zinazofanywa na mamlaka, tutatoa maagizo siku ambayo tutaitembelea,” alisema Bukwimba.
Hata hivyo, mwenyekiti wa Bodi ya TCRA, Profesa Haji Semboja aliitetea mamlaka hiyo akisema kiasi hicho kilichotumika kwa ajili ya semina, mafunzo na warsha kinatokana na unyeti wa taasisi hiyo.
“Taasisi inasimamia kampuni zinazotoa huduma za teknolojia za kisasa ambayo ni ngeni hapa kwetu, hivyo wafanyakazi wetu wanatakiwa kuwa na ufahamu zaidi ya hao watoa huduma,” alisema Profesa Semboji.
Semboja, ambaye ni mchumi, alisema: “Pamoja na mambo mengine, wafanyakazi wetu wanasimamia kampuni za mitandao ya simu, matoleo ya simu yanatoka mara kwa mara, wanatakiwa kufahamu teknolojia wanayoisimamia. Hapa ni lazima waende darasani.”
Alisema wafanyakazi hao wakiachwa bila kupata mafunzo ya mara kwa mara watajikuta baada ya kipindi kifupi wanapitwa na teknolojia zinazozidi kuibuka kila wakati.
Kwa upande wake, Sabrina Sungura ambaye ni mjumbe na mbunge wa Viti Maalumu, aliitaka mamlaka hiyo kufanya marekebisho ya minara ya simu mkoani Kigoma.
“Hii ni hatari kwa usalama,” alisema.
0 comments:
Post a Comment