Wabunge wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara wamemtaka Rais John Pombe Magufuli kulitumbua jipu shirika la umeme Tanesco kwa kununua transfoma kutoka nje ya nchi licha ya kumiliki asilimia 20% ya hisa katika kiwanda cha Tansfoma cha Tanalec kilichopo jijini Arusha .
Kamati hiyo ya Bunge imebaini hayo wakati wa ziara yao ya kutembelea viwanda jijini Arusha ili kufahamu changamoto na kasi ya ukuaji wa viwanda ambapo Wabunge hao wameshangazwa na kitendo cha Tanesco kutonunua transfoma katika kiwanda hicho ambazo huuzwa katika nchi jirani za Kenya ,Zambia Malawi na Burundi.
Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema ambaye ni Mjumbe wa Kamati hiyo alisema kuwa ni jambo la kushangaza kwa Tanesco ambao ni wamiliki wa Tanalec na wako katika wakurugenzi wa bodi lakini bado wanaagiza transfoma nje ya nchi suala ambalo linapaswa kutazamwa kwa umakini na kupatiwa majibu.
“Tunashindwa kuilewa Tanesco kwanini wanafanya hivyo wakati kiwanda ni cha kwao na wakati Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco Felchesmi Mramba yuko ndani ya bodi ya wakurugenzi ,hapa kuna mgogoro ambao unapaswa kuatatuliwa kwa wakati ili kunusuru kiwanda hiki” Alisema Lema
Naye Mbunge wa Singida Mjini Musa Sima wamesema kuwa uamuzi huo wa Tanesco kununua transfoma za nje ya nchi unazorotesha ukuaji wa viwanda vya ndani na kukiuka adhma ya Rais Magufuli ya kujenga uchumi wa viwanda nchini kwani ni vigumu kukuza viwanda wakati bila kuvilinda viwanda vya ndani dhidi ya bidhaa za nje.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Vicky Kamata na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dalali Kafumu wameitaka serikali kuchukua maamuzi juu ya suala hilo la Tanesco ili kulinda viwanda vya ndani viweze kuchochea maendeleo ya Taifa.
Meneja Mkuu wa Tanaleck Zahir Salehe ameiomba serikali irekebishe sheria za manunuzi ili zitoe kipaumbele kwa viwanda vya ndani viweze kukua na kutoa ajira nyingi hivyo kukuza pato la nchi.
0 comments:
Post a Comment