Katibu Mkuu Kiongozi John Kijazi
Wakuu hao wa wilaya na wakurugenzi wao walikuwa waondoke jana kwa ufadhili wa Serikali ya Watu wa China, lakini habari zinaarifu kuwa Ikulu iliamua kutotoa kibali, hali inayozidisha ubashiri kuwa uamuzi huo umetokana na kukamilika kwa uteuzi wa wakuu wapya.
Safari hiyo ilishakamilika kwa kiwango kikubwa baada ya kupata visa na wengi wao kuwasili jijini Dar es Salaam tayari kwa safari hiyo, lakini wakalazimika kurejea kwenye vituo vyao baada ya kukosa kibali cha Ikulu ambacho hutolewa na Katibu Mkuu Kiongozi.
Mara tu baada ya kuapishwa Novemba 5 mwaka jana, Rais John Magufuli alitangaza kudhibiti safari za nje za watumishi na viongozi wa umma kwa kuagiza kuwa Ikulu ndiyo itakayotoa kibali baada ya kujiridhisha na umuhimu wa safari hizo kwa Taifa.
Tangu atoe agizo hilo, ni mawaziri wawili tu ambao wameruhusiwa kwenda Vietnam kwenda kujifunza kilimo na viwanda. Mawaziri hao ni Mwigulu Nchemba (Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi) na Charles Mwijage (Viwanda na Biashara).
Naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji alikwenda nchini Ethiopia kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa fedha, wakati kwa nyakati tofauti Makamu wa Rais Samia Suluhu na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa walikwenda Afrika Kusini na Botswana.
Mpaka sasa, Rais Magufuli amefanya safari moja tu ya nje alipokwenda Rwanda kwenye maadhimisho ya mauaji ya kimbari.
Lakini safari ya wakuu hao wa wilaya ilikuwa ifadhiliwe na China, kwa mujibu wa habari hizo na hivyo isingeisababishia Serikali kutumia vibaya fedha za walipa kodi.
Uamuzi huo unaonekana kuzingatia zaidi uteuzi wa wakuu wapya ambao taarifa zinasema unaweza kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa, wakati wa wakurugenzi wa wilaya unatazamiwa kutangazwa baadaye wiki hii au wiki ijayo.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alikiri kuwapo kwa safari hiyo, lakini akasema hajui kama imeidhinishwa na Ikulu kwa kuwa si muhusika.
“Katika hatua za awali nilisaini safari hiyo kuwaruhusu waende China, lakini sijui kama wamenyimwa kibali kwa sababu hilo si suala la ofisi yangu,” alisema Waziri Simbachawene.
Kama ni kweli, alifafanua Simbachawene, inaweza kuwa ni kutokana na umuhimu wao wa kuwatumikia wananchi kwenye maeneo wanayotoka. “Hawawezi kuondoka na kuziacha wilaya zao ilhali wao ndiyo waangalizi,” alisema Simbachawene.
Akiwa Chato mkoani Geita, Rais aliwataka wakuu wa wilaya kuchapa kazi badala ya kuwa na woga wa kutoteuliwa akisema uchapaji kazi ndio utawafanya waendelee kuwapo kwenye nafasi zao.
Rais pia amekuwa akitoa maelezo kadhaa yanayoonyesha atafanya uteuzi kwa kutumia vigezo hivyo, hasa suala la elimu ambayo inakabiwa na tatizo kubwa la uhaba wa madawati na vyumba na majengo, kipindupindu, njaa, migogoro ya ardhi na watumishi hewa
0 comments:
Post a Comment