Latest News
Loading...

Mbunge wa Zamani na Moshi Vijijini (CCM) Apandishwa Kizimbani


Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Thomas Ngawaiya amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na shtaka la kujenga hoteli kwa kutumia makandarasi wasiosajiliwa.

Ngawaiya ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Moshi Vijijini na pia Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Kilimanjaro, alipandishwa kizimbani jana na kusomewa shtaka hilo, siku moja baada ya kutiwa mbaroni na Polisi Kinondoni.

Kabla ya kumsomea shtaka, Mwendesha Mashtaka kutoka Bodi ya Usajili wa Makandarasi (ERB), Saddy Kambona alisema Ngawaiya amefikishwa mahakamani hapo kwa kukaidi amri ya Mahakama.

Pia, Wakili Kambona alimsomea mshtakiwa huyo shtaka linalomkabili, lakini Ngawaiya alikana na kuachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti.

Wakili Kambona alidai kuwa Machi 24, 2015 majira ya mchana, mshtakiwa alitenda kosa la kuagiza ujenzi wa jengo la hoteli, kwa watu ambao hawajasajiliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi.

Alidai kuwa jengo hilo lipo Kiwanja Namba 32, makutano ya mitaa wa Dosi na Wazani, eneo la Magomeni Mapipa, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Aliendelea kudai kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume cha kifungu namba 22 cha Sheria ya Bodi Usajili wa Makandarasi, Namba 17 ya Mwaka 1997.

Akitoa ufafanuzi nje ya Mahakama, Wakili Kambona alibainisha kuwa sheria hiyo inamtaka kila anayejenga jengo ambalo ni kwa matumizi ya umma lazima atumie makandarasi waliosajiliwa na ERB.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, kisha kuulizwa na Hakimu Hellen Liwa iwapo ni kweli au la, Ngawaiya alianza kujitetea.

Hakimu Liwa alimzuia na kumtaka ajibu shtaka kabla ya Wakili wake, Desidery Ndibalema kuingilia kati na kumuelekeza kwa kumnong’oneza cha kufanya, ndipo akakanusha shtaka.

Wakili Kambona baada ya kumsomea mshtakiwa shtaka hilo, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na kuomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa. Hakimu Liwa aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili, 11.

0 comments:

Post a Comment