Latest News
Loading...

Rais Magufuli Awataka Mawaziri wasioweza Kazi Bila Posho au Safari Wajiondoe Wenyewe

 
Viongozi  serikalini wakiwemo mawaziri na makatibu wakuu, wameombwa na Rais John Magufuli, kuvumilia machungu wakati wa uongozi wake, kama ambavyo wananchi walivyovumilia tangu Uhuru.

Amesema hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya kwanza ya juu (flyover) nchini Tanzania, inayojengwa katika makutano ya Barabara ya Mandela na Barabara ya Nyerere, eneo la Tazara, kwa ufadhili wa Serikali ya Japan. 
Machungu hayo kwa mujibu wa Rais Magufuli, yataanza kuonekana wakati wa utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ya kwanza kwa Awamu ya Tano, ambayo fedha za maendeleo zimeongezeka kutoka asilimia 27 za bajeti iliyopita, hadi kufikia asilimia 40.

Machungu yenyewe 
Ili kufanikisha dhamira hiyo ya Serikali, Rais Magufuli alisema katika bajeti hiyo inayotarajiwa kupelekwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, litakaloanza vikao vyake Dodoma wiki ijayo, machungu hayo yataanza kuonekana kwani fedha za chai, semina na safari, zimekatwa na kujaziwa katika fedha za maendeleo.

Kutokana na makato hayo, Dk Magufuli amesema kutakuwa na machungu hasa kwa watendaji wa Serikali na kuwaomba mawaziri na makatibu wakuu ambao alisema walikuwa wakifaidi matunda ya Uhuru, wavumilie machungu hayo kwani wananchi wa maisha ya chini wamevumilia machungu kwa muda mrefu.

“Wananchi wamechoka kutuona sisi viongozi tunafaidi matunda ya Uhuru wa nchi tangu Uhuru na wao wakiwa wasindikizaji halafu wao tunawaomba kura na wakishatupigia tunawasahau,” alisema na kuongeza kuwa anataka wananchi watoke kwenye machungu na sasa wawe ‘watamu’ kwa maendeleo.

Magufuli alisema lazima viongozi wabadilike na kurudi kwa wananchi wa maisha ya chini na hiyo itakuwa sadaka kwa kuwapa madaraka kwani wananchi wanyonge wameteseka siku nyingi.

Wasiovumilia 
Alisema waliokuwa wamezoea chai, safari na posho za ovyo kama wanaona au wanafikiri hawawezi kufanya kazi bila hizo chai, waache kazi mara moja kwani sasa fedha zinazokusanywa za walipa kodi wanyonge, zitaenda kutatua matatizo yao ya hospitali, barabara na kununua ndege za Serikali.

Pia alionya kuwa katika uongozi wake hakuna mtu atakayekwenda kinyume na utaratibu na kisha ‘akachomoka salama’ na kama kuna anayeona hawezi ajiondoe mwenyewe kwani Watanzania wanaendelea kumuombea.

Dk Magufuli alisema wananchi wote bila kujali vyama vya siasa, wanalilia maendeleo na maendeleo hayana chama, kwani wananchi wamechoka ‘machama chama’, wanataka kwenda mbele, hivyo hakuna sababu ya kubaki nyuma na kubishana kwa mambo ya chama chama, wakati uchaguzi umepita na aliyeshinda ni yeye ambaye ni CCM.

Machungu ya zamani 
Ingawa Rais Magufuli alisema machungu hayo yataanza kuonekana katika Bajeti inayotarajiwa kuanza kujadiliwa na Bunge litakaloanza vikao wiki ijayo, lakini watendaji wa Serikali walianza kuona machungu ya msimamo wake tangu alipoingia madarakani Novemba mwaka jana.

Itakumbukwa kuwa Novemba 7, mwaka jana akiwa Ikulu, Dar es Salaam, katika mkutano wake wa kwanza na watumishi wa ngazi za juu wa Serikali, hasa makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu na watendaji wengine wakuu wa Serikali, Rais Magufuli alitangaza kufuta safari zote za nje ya nchi hadi hapo atakapolitolea suala hilo uamuzi mwingine.

Mpaka sasa Rais Magufuli amehakikisha shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi zinafanywa na kusimamiwa na mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha nchi, ambapo watumishi watasafiri nje iwapo kutatokea jambo la dharura na pamoja na udharura wake, lazima kibali kitolewe na yeye, Katibu Mkuu Kiongozi au Makamu wa Rais.

Katika kile kinachoonekana kuwa hatanii, Rais Magufuli aliagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa watumishi waandamizi wanne wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ambao walikaidi agizo lake la kuwataka watumishi wa umma kutosafiri nje ya nchi.

Watumishi hao ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nikitas ambao walisafiri kwenda nje ya nchi, licha ya kutokuwa na kibali cha safari kutoka kwa Rais ama Katibu Mkuu Kiongozi.

Aidha ndani ya siku zake 100 za kwanza tangu alipoingia madarakani, tayari Serikali yake ilikuwa imeshawafukuza kazi vigogo zaidi ya 70 kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo za ufisadi.

Novemba 9, mwaka jana, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Sefue, alitangaza kuwa Rais Magufuli aliamua kufuta shamrashamra za Sikukuu ya Uhuru ambapo fedha zilizookolewa aliagiza zipelekwe katika mradi wa kupanua kipande cha barabara kutoka Morocco mpaka Mwenge katika wilaya ya Kinondoni.

Hatua hiyo ilitanguliwa na kupunguza fedha za sherehe ya kupongezana ya wabunge, ambazo alizielekeza kwenda kununua vitanda, magodoro na mashuka kwa ajili ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Hivi karibuni alipokuwa akiapisha wakuu wa mikoa, aliwataka kwenda kuwasaka watumishi hewa na kutangaza idadi yao, ambapo aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela, aliposema hajakuta watumishi hewa wakati wapo, Dk Magufuli hakusita kumuondoa mwanzoni mwa wiki hii, ingawa hakuwa amemaliza hata mwezi tangu aripoti kazini

0 comments:

Post a Comment