Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, amekionya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuhusu mikutano ya hadhara na maandamano yanayotarajia kuanza Septemba 1 mwaka huu.
Alhamis hii, Mwenyekiti wa Chadema taifa, Freeman Mbowe alitangaza maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyoketi kwa dharura huku kufanyika kwa mikutano ya hadhara na maandamano kote nchini kuanzia Septemba 1.
Mbowe aliwataka viongozi wa Chadema katika ngazi zote hapa nchini, wabunge na madiwani kufanya maandalizi ya mikutano na maandamano huku pia akitangaza kuanzishwa kwa Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (UKUTA).
Hata hivyo, Jaji Mtungi mapema hii leo amevieleza vyombo vya habari kuwa, “tamko la Chadema limejaa lugha ya uchochezi, kashfa, linaloudhi na lenye kuhamasisha uvunjifu wa amani.”
Pia amewaeleza kuwa sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992 katika kifungu cha 9 (2) (c) inakataza chama chochote cha siasa hapa nchini kutumia na kuhamasisha matumizi ya nguvu au vurugu kama njia ya kufikia malengo yake kisiasa.
“Si hayo tu, bali pia kifungu cha 9 (2) (f) kinakataza chama cha siasa kuruhusu viongozi au wanachama wake kutumia lugha ya matusi, kashfa na uchochezi ambao unaweza kusababisha kutokea kwa uvunjifu wa amani,” amesema Jaji Mutungi.
Mvutano baina ya Chadema na jeshi la polisi juu ya kufanyika kwa mikutano ya hadhara umekuwa ukiendelea kwa muda sasa, kufuatia jeshi hilo kutoa tangazo la kuzuia mikutano ya hadhara Juni mwaka huu kwa madai ya kuwepo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani.