Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya aliondoka nchini mwake jana asubuhi kwenda Ufaransa na Ujerumani kwa ziara ya kazi ambayo pamoja na mambo mengine itahusisha suala la ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda.
Kenya hivi karibuni imeingia katika mvutano na Uganda, ikiitaka jirani yake huyo kurudisha mpango wa kulipitisha bomba hilo la mafuta nchini humo (Kenya) badala ya Tanzania.
Suala hilo ni sehemu ya ajenda ya biashara, ushirikiano na maendeleo ambayo ni moja ya malengo ya ziara ya Rais Kenyatta.................
Kituo cha kwanza cha ziara ya Rais Kenyatta kitakuwa Paris, Ufaransa, kuanzia leo Aprili 4 hadi 6 kabla ya kuelekea Berlin, Ujerumani atakakokaa hadi Aprili 8, mwaka huu.
Itakuwa ni mara ya kwanza katika miaka 17 kwa Rais wa Kenya kuitembelea Ujerumani.
Mara ya mwisho, ziara ya aina hiyo ilifanywa na Rais Daniel arap Moi mwaka 1999 huku Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, akiitembelea Kenya mwaka 2011.
Ziara nchini Ufaransa kwa mujibu wa Ikulu ya Kenya, imeandaliwa na wizara ya mambo ya nje kwa mwaliko wa Rais François Hollande.
Ziara ya Ufaransa inatarajia kuipa Kenya fursa ya kuzungumzia suala la ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda, ikilenga kuiomba serikali ya nchi hiyo kutia mkono wake kufanikisha azma yake ya ujenzi wa bomba hilo. Kenye inahesabu imeporwa na Tanzania mradi huo.
Kampuni ya Total ya Ufaransa ni mwanahisa mkubwa wa uwekezaji wa mafuta Uganda na inaaminika ndiyo iko nyuma ya uamuzi wa hivi karibuni wa Uganda kuachana na mpango wa ujenzi wa bomba hilo kutoka njia ya Hoima- Lokichar- Lamu ya Kenya na badala yake kulijenga hadi katika bandari ya Tanga, Tanzania.
Tofauti na washirika wengine wa uwekezaji huo kutoka Uingereza na China, Total mara kwa mara imekuwa ikisisitiza ujenzi wa bomba hilo kupitia njia ya Kusini nchini Tanzania kwa kile inachosema unafuu na usalama kulinganisha na Kenya.
Tayari mmoja wa viongozi wake waandamizi amemtembelea Rais John Magufuli Ikulu, Dar es Salaam na kumhakikishia dhamira ya kampuni hiyo pamoja na kupatikana kwa fedha za ujenzi huo.
Kampuni hiyo pia imetoa tamko jingine hivi karibuni wakati wa mkutano wa wadau wa nishati Afrika Mashariki uliofanyika Dar es Salaam, ikisema inajua jitihada zinazofanywa na Kenya kutaka bomba hilo lijengwe nchini humo, lakini msimamo wake wa kujengwa Tanzania uko pale pale.
Kwa mujibu wa taarifa za Ikulu, Ufaransa iko katika nafasi ya sita kama mmoja wa wawekezaji wakubwa Kenya.
Uwekezaji huo unaanzia sekta ya uchukuzi, ufamasia, magari na sekta ya huduma zikiwamo SDV-Transami, AGS, Frasers Schneider, Peugeot, Renault, Michelin na Proparco.
Wawekezaji wengine ni Total Kenya, Bamburi Cement, Alcatel, na kampuni ya mawasiliano ya Ufaransa Telecom yenye ubia na Telkom Kenya na Orange Mobile.
Kwa mujibu wa mpango wa ziara nzima, Rais Kenyatta akiwa Ujerumani atakuwa na mkutano na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel.
Miongoni mwa masuala ya kujadiliwa nchini humo ni pamoja na biashara, uwekezaji na ushirikiano katika usalama, utamaduni na elimu, utalii, amani katika kanda na migogoro ya Sudan Kusini na Burundi.
Latest News
Loading...
Home »
KIMATAIFA
» Uhuru Kenyatta Ashupalia Ujenzi wa Bomba la Mafuta Toka Uganda hadi Tanzania.....Aenda Ufaransa kukutana na viongozi wa Total Ili Kuwaomba Lipite Kenya
0 comments:
Post a Comment