Mbunge wa Muleba Kusini Profesa Anna Tibaijuka ametunukiwa tuzo ya heshima ya Maendeleo Endelevu ya Mwana Mfalme Khalfa bin Salman Al Khalifa ikiwa ni utambuzi wa mchango wake wa kuchochea maendeleo
Tibaijuka ameyasema jana wakati akizungumza na wanahabari kwa lengo la kuelezea namna alivyopatiwa tuzo hiyo pamoja na fedha kiasi cha dola laki moja ambayo amekataa kuichukua kutokana na hofu ya kukumbwa na kashfa kama ile iliyomkumba wakati akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika serikali ya awamu ya nne.
Pia alisema kuwa tuzo hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Bahrain na hutolewa baada ya miaka miwili kwa mtu ambaye ametoa mchango mkubwa katika kutatua changamoto za sekta mbalimbali za kiuchumi ambazo zinawakumba wananchi.
Profesa Tibaijuka alifafanua kuwa tuzo hiyo imetokana na kushughulikia malengo ya milenia wakati akiwa anafanya kazi katika Umoja wa Mataifa (UN) na kusema kuwa tuzo hiyo ni heshima kwa watanzania kwani alienda kuwawakilisha kwenye umoja huo.
0 comments:
Post a Comment